“Kila kilichoumbwa katika ulimwengu mzima siyo kingine ila mlango unaoongoza kwenye ujuzi Wake…”— Bahá'u'lláh
Maandiko ya Kibahá’í hueleza kwamba asili ya Mungu huzidi uelewa wa akili yoyote ya binadamu, ingawa twaweza kupata vielelezo vya sifa Zake katika kila kitu kilichoumbwa. Tangu zama za kale, Ametuma mfuatano wa Mitume Watakatifu, wanaojulikana kama Wadhihirishaji wa Mungu, kuelimisha na kuongoza wanadamu, wakiamsha katika watu wote uwezo wa kuchangia kwenye uendeleaji wa ustaarabu kwa kiasi ambacho haikuwezekana kabla.
Mungu, Muumbaji wa ulimwengu, ni ajuaye yote, mwenye upendo wote na mwenye rehema yote. Kama vile jua la kimwili linavyoangazia dunia, hivyo ndivyo mwanga wa Mungu humiminwa juu ya muumbo wote. Kupitia mafundisho ya Wadhihirishaji wa Mungu—miongoni mwao Ibrahimu, Krishna, Zoroasta, Musa, Buddha, Yesu Kristo, Muhammad, na, hivi karibuni, Báb na Bahá’u’lláh—uwezo wa kiroho, wa kiakili na wa kimaadili wa binadamu umekuzwa.
Uzuri, utajiri na anuwai ya ulimwengu wa asili vyote ni vielelezo vya sifa za Mungu. Hii huamsha ndani mwetu heshima ya kina kwa mambo ya asili. Binadamu huwa na uwezo kujikomboa kutoka ulimwengu wa asili na, kama mlinzi wa asilimali kubwa mno za sayari, ni mwenye madaraka kutumia malighafi za sayari katika namna ambayo huhifadhi upatano na huchangia kwenye maendeleo ya ustaarabu.
Binadamu, baada ya kupitia umri wa uchanga na utoto, sasa husimama kwenye kizingiti cha ukomavu wake wa pamoja, ambao sifa yake bainifu itakuwa kuunganishwa kwa binadamu wote katika ustaarabu wa kiulimwengu. Kuibuka kwa ustaarabu huu, wenye usitawi katika mielekeo yake yote miwili ya kiroho na ya kimwili, humaanisha kwamba vipengele vya kiroho na vya kiutendaji vya maisha ni vya kusogea mbele pamoja kwa upatano.