Vitendo vya ibada ni sehemu ya asili ya maisha ya kidini. Kupitia kwavyo, watu binafsi na jumuiya huendelea kuimarisha fundo la kipekee lililopo kati ya Mungu na binadamu . Fundo hili huyapa nguvu mahusiano ambayo hudumisha jamii—kati ya watu binafsi na miongoni mwa vipengele mbalimbali vya jumuiya na asasi zake.
Sala ni muhimu kwa ajili ya uhai na ukuaji wa roho zetu. Kupitia kwayo tunaweza kumtukuza Mungu na kuonesha upendo wetu Kwake, vile vile kumuomba msaada Wake. Uwezo wa kutafakari ni sifa bainifu ya binadamu. Haswa, maandiko ya Kibahá’í hupendekeza kuwa maendeleo ya binadamu hayawezekani bila kutafakari na kufikiri kwa kina. Mfungo na hija ni vitendo vingine viwili ya kiibada ambavyo huchukua nafasi ya muhimu katika maisha ya kiroho katika vipindi vyote vya historia ya binadamu. Kazi inaweza pia kuchukuliwa kama kitendo cha ibada pale inapofanywa katika moyo wa huduma.
“Kusanyikeni kwa pamoja kwa shangwe kamili na urafiki na mseme aya zilizofunuliwa na Bwana wa ukarimu. Kwa kufanya hivyo milango ya maarifa ya ukweli itafunguliwa kwa nafsi zenu za ndani, na ndipo mtahisi roho zenu zikijazwa na uthabiti na mioyo yenu kujazwa na shangwe ing’arayo.”
— Bahá'u'lláh