Mafundisho ya Bahá’u’lláh ni mapana mno katika wigo wao, yakichunguza kama yafanyavyo mawazo kama asili na dhumuni la Ufunuo, ubora wa kiasili wa wanadamu, uendelezaji wa sifa za kiroho, na mwingiliano wa binadamu na ulimwengu wa asili. Maandiko ya Kibahá’í yamejawa na marejeo kwenye amani ya ulimwengu—”lengo kuu kabisa la binadamu wote”—pamoja na maelezo kuhusu kanuni za kijamii zinazohusiana na amani hii.
Miongoni mwa kanuni hizi ni utafutaji unaojitegemea wa ukweli; umoja wa jamii nzima ya binadamu, ambayo ni kanuni ya kimsingi ya Imani ya Kibahá’í; uondoaji wa aina zote za hisia za chuki au mapenzi ya bila sababu; upatano ambao lazima uwepo kati ya dini na sayansi; usawa wa wanaume na wanawake, mabawa mawili ambayo kwayo ndege wa binadamu huweza kuruka; uanzishwaji wa elimu ya lazima; kutwaa lugha saidizi ya kiulimwengu; uondoaji wa utajiri na umaskini wa kupita kiasi; kuwekwa kwa mahakama ya dunia kwa hukumu ya migogoro kati ya mataifa; na kuithibitisha haki kama kanuni inayotawala katika masuala ya kibinadamu. Wabahá’í hawaoni kanuni hizi kama matamko tu ya matamanio matupu—zinaeleweka kama masuala yenye uhitaji wa umakini wa haraka na wa kivitendo kutoka kwa watu binafsi, jumuiya, na asasi hali kadhalika.
Mnamo Oktoba 1985, Nyumba ya Haki ya Ulimwengu ilitangaza uchapishwaji wa barua iliyoandikwa kwa wanadamu kwa ujumla juu ya mada ya amani ya ulimwengu, kwa jina “Ahadi ya Amani ya Ulimwengu”. Ikieleza mantiki za kimsingi za matumaini ya jumuiya ya Kibahá’í kuhusu ujio wa amani ya kimataifa kama ngazi inayofuata katika mabadiliko endelevu ya jamii, ilieleza wazi:
Amani Kuu ambayo kuelekea kwake watu wa nia njema kupitia karne zote wamekuwa wakielekeza mioyo yao, ambayo manabii na washairi kwa vizazi visivyohesabika wameelezea maono yao, na kwayo toka wakati hadi wakati maandiko matakatifu ya binadamu wakati wote yameiendeleza ahadi, hivi sasa hatimaye ipo karibu na uwezo wa kufikia wa mataifa. Kwa mara ya kwanza katika historia inawezekana kwa kila mmoja kuiona sayari nzima, pamoja na idadi kubwa mno ya watu wake na tofauti zao mbalimbali, katika mtazamo mmoja. Amani ya ulimwengu sio tu kwamba inawezekana lakini haiepukiki.